Klabu ya Arsenal imefungua msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza maarufu kama EPL kwa kishindo kwa kuwatandika wenyeji Crystal Palace 2-0 katika uwanja wa Selhurst Park.
Baada ya kukosa dakika za mwisho nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa msimu huu, the Gunners walielekea sokoni kutafuta vifaa vya kuwafaa msimu huu na dalili zinaonekana.
Arsenal pia walijibidisha katika mazoezi ya maandalizi ya msimu waking’aa katika mechi mbalimbali ikiwemo ile waliyompiga Chelsea 4-0 nchini Marekani. Usiku wa Ijumaa, Agosti 5, ilikuwa nafasi ya
Arsenal kufungua msimu wa 2022/23 kwa kuwatembelea Crystal Palace ambao wananolewa na nahodha wao wa zamani Patrick Vieira.
Tofauti na ilivyokuwa msimu jana ambapo Arsenal walianza kampeni yao kwa kulazwa 2-0 na vijana wapya Brentford na kushikilia mkia, Arsenal waliwalima Palace 2-0 na kupanda hadi nafasi ya kwanza kwenye jedwali.
Oleksandr Zinchenko na Gabriel Jesus ambao walitwaaliwa kutoka Manchester City mwezi jana walianza mchezo huo huku pia William Saliba akipata nafasi ya kuchezea the Gunners kwa mara ya kwanza baada ya kuhudumu nchini Ufaransa kwa mkopo.
Gabriel Martinelli aliwapa the Gunners uongozi katika dakika ya 20 baada ya kupakuliwa pasi ya hewani na Zinchenko huku beki Marc Guehi akijifunga katika dakika ya 85 na kuwahakikisha Arsenal ushindi wa 2-0.
Arsenal sasa inaongoza jedwali kwa alama tatu na mabao mawili huku Palace ikiwa ya mwisho.
Liverpool, Chelsea na Tottenham zinashuka uwanjani Jumamosi huku Manchester United na Manchester City zikiwa na kibarua Jumapili.
Ratiba kamili ya mechi za ufunguzi wa msimu
Ijumaa, Agosti 5
Crystal Palace v Arsenal
Jumamosi, Agosti 6
Fulham v Liverpool
Bournemouth v Aston Villa
Leeds United v Wolverhampton Wanderers
Everton v Chelsea
Newcastle United v Nottingham Forest
Tottenham v Southampton
Jumapili, Agosti 7
Leicester City v Brentford
Manchester United v Brighton
West Ham United v Manchester City
0 Comments