Ticker

6/recent/ticker-posts

"Terry alinikatia simu mara ya kwanza nilipo mpigia kumuomba idhini ya jezi 26" - Koulibaly

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


Mchezaji sajili mpya wa miamba wa Uingereza Chelsea, Kalidou Koulibaly katika mahojiano ya kipekee na timu hiyo baada ya kukabidhiwa jezi nambari 26 mgongoni alifunguka kwamba mchezaji mkongwe John Terry ambaye aliivalia jezi hiyo kwa muda mrefu kama nahodha mara ya kwanza alimkatia simu alipompigia kumuomba idhini ya kutumia jezi hiyo.

Jarida la Mirror linaripoti kwamba Koulibaly alisema mara ya kwanza alipompigia simu Terry kumuomba idhini ya kutaka kutumia jezi nambari 26, Terry alikata simu akifikiria ni mtu mwingine anamfanyia utani na baadae kumpigia kocha wa timu ya Chelsea kumuuliza nini kilikuwa kinaendelea.

Koulibaly alinukuliwa akisema kwamba alizungumza na kiungo mshambulizi Muitaliano Gian Franco Zola ambaye aliitumikia Chelsea miaka ya mapema 2000 na kumuelezea historia ya timu hiyo ambapo alimpa namba ya Terry ili wazungumze amuulize kama anaweza tumia jezi nambari 26 ambayo ilifahamika kwa miongo kadhaa kuwa ya Terry.

“Nilimuuliza Gianfranco Zola, ambaye alinieleza historia ya Chelsea na kunipa namba ili nimpigie John nimuombe jezi. Alinipa namba na nikampigia. Mwanzoni hakuamini kuwa ni mimi, aliona ni mzaha, alimpigia simu meneja wa timu kumuuliza kama ni mimi, najua ni namba muhimu... aliponiambia ‘ndio’ nilimpigia simu. Alikuwa na furaha sana. Najua alichofanya kwa klabu na wafuasi wake." Alisema Koulibaly kama alivyonukuliwa na Mirror.

Jezi nambari 26 haijawahi kuvaliwa tena tangu mwaka 2017 John Terry alipoondoka katika klabu ya Chelsea na ni moja ya jezi zinazosheheni heshima zilizotukuka kutokana na mchezaji huyo kuivalia vizuri na kushinda mataji ya kutukuka, kando na kuwa nahodha kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Koulibaly pia ana utashi na mapenzi na jezi hiyo ambayo kwa miaka 8 aliyoitumikia Napoli ndio ilikuwa jezi yake na ndio maana alipoingia Chelsea alitaka kujua nani anaitumia kabla ya kumuomba idhini ya kuitumia.

Post a Comment

0 Comments