Ticker

6/recent/ticker-posts

Zoran Maki Ataka Wapinzani Wajipange

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

BAADA ya kutambulishwa kocha mkuu wa Simba, Zoran Maki amewataka wapinzani wake wajipange kwani yuko tayari kwa kazi.

Zoran amesaini mkataba wa mwaka mmoja akichukuwa nafasi ya Mhispania Pablo Franco, amesema kwamba kipaumbele chake ni kufanya kitu cha tofauti na Simba Kuelekea msimu ujao.


Amesisitiza kwamba anataka kufanya makubwa zaidi ya alivyofanya kwenye Ligi za Sudan, Morocco na Algeria ambako ni kugumu kama Tanzania lakini ametamba pia haihofii dabi ya Agosti 13 dhidi ya Yanga kwavile amezoea mechi kama hizo.

Akizungumza wakati wa utambulisho wake, Zoran alisema; "Nilicheza mechi 15 ndani ya miezi miwili na isitoshe ningekuwa Ulaya ningepewa miaka minne ila huku ni tofauti hivyo nina uzoefu na soka la Afrika na hakuna shida juu ya hilo kwani jambo kubwa ni ushirikiano."

"Siwezi kutoa ahadi kubwa kwenye michezo ya kimataifa ingawa ninachotaka ni kufanikisha mambo, tuwe na mwenendo mzuri kwenye michuano mbalimbali na kurejesha heshima ya Simba ambayo msimu uliopita ilikosekana," alisema.

"Nataka kufanya vizuri zaidi ya huku nilikotoka na hili linawezekana kama tukiwa na ushirikiano mzuri, Simba ni klabu kubwa Afrika hilo halipingiki,"aliongeza na kusisitiza kwamba anatamani kucheza zaidi ya nusufainali ya Afrika alikofika na Wydad Casablanca.

Zoran aliongeza kuwa ligi ya Tanzania ni nzuri na yenye ushindani akiifananisha na ya Angola kwani asilimia kubwa mabingwa ni wale wale waliozoeleka tofauti na nchi za Morocco na Algeria ambazo zinaweza kutoa bingwa yoyote.

Kuhusu mkataba wake, Zoran alisema kupewa mkataba wa mwaka  mmoja sio kitu kibaya kwake kwani sehemu zingine wanatoa mkataba wa miezi sita.

“Nina uzoefu wa soka la Afrika huwa wanatoa mkataba wa miezi sita, huu wa mwaka mmoja ni mzuri japokuwa itanichukua hata miezi sita kwanza kujua namna ambavyo soka la hapa linavyokwenda,” alisema Zoran.

Zorani alisema anaifahamu Simba baada ya kuiona kwenye mashindano ya CAF na hata aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Didier Gomes alikuwa anamfuatilia vizuri.

“Naijua Simba kwa sababu nimeona mechi zao za CAF, Yanga naijua kidogo sana maana sijawahi kuona mechi zao, Kocha wa zamani Simba, Didier nilikuwa naye Ligi ya Sudan na nilimfunga ila ni kocha mzuri sana,” alisema Zoran ambaye amewahi kuzifundisha timu za Wydad Ac (Morocco), Al Hilal (Sudan) na CR Belouizdad .

Naye Meneja Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema viongozi wao wote walijiridhisha juu ya ubora na uzoefu wa kocha huyo hasa soka la Afrika kitu ambacho ndicho kigezo kikuu kilichozingatiwa katika kumuajiri.

Miongoni mwa malengo aliyopewa kocha huyo ni kuhakikisha timu inachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao iliukosa msimu ulioisha, kuchukua Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kuifikisha hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya kutua nchini zoran atajiunga na kikosi hicho kwenye maandalizi ya msimu mpya wakati kitakaposafiri Julai 14 kwenda Misri ili kuweka kambi huku mtihani wake wa kwanza ni dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii Agosti 13.

Kuhusu safari yao ya Misri, Ahmed alisema; “Tunaondoa Julai 14 mwezi huu na tutakuwa hadi Agosti 8 tutarudi kwa ajili ya Simba Day pamoja na mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi, “Tutakuwa na wachezaji wote kasoro wale ambao watakuwa kwenye timu za Taifa ambao tutawaacha wakiwa na majukumu mengine.” alisema na kuongeza; “Zoran yupo hapa kuhakikisha Simba inapata ubingwa wa Ligi, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho pamoja na kuingia nusu fainali Caf,” alisema Ahmed.

Post a Comment

0 Comments