Ticker

6/recent/ticker-posts

TFF Yamfungia Manara miaka miwili, faini ya Sh20 milioni

KAMATI ya Maadili ya TFF, imemfungia Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara kutojihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili na faini ya Sh20 milioni kwa kosa la kumtolea maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Wallace Karia katika mechi ya fainali ya kombe la Azam iliyopigwa Jijini Arusha.

Manara amepatikana na hatia hiyo ya kumtishia na kumdhalilisha Karia siku ya Jumamosi Julai 2, 2022 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakati wa mechi ya fainali kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union.

Akizungumzia hilo katibu wa kamati ya maadili ya shirikisho hilo, Walter Lungu alisema kamati hiyo ilikutana  kuanzia Julai 11 mwaka huu katika ofisi za Shirikisho hizo zilizopo maeneo ya Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Lungu alisema katika kikao hicho ilipitia malalamiko yaliyoletwa na Sekretarieti ya TFF kumuhusu Haji Manara inayohusu mienendo ya tabia na maadili kifungu cha 73 ibara ya (5) ya mwaka 2021.

Akisoma hukumu hiyo, Lungu alisema katika mchezo huo, Manara alitoa maneno yasiyofaa mbele ya Rais Karia huku akinukuu maneno hayo kwa kusema " “Wewe unanifatafata sana, hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote,kwa chochote na huwezi kunifanya chochote. Nina uwezo wa kukufanya chochote na huna cha kunifanya.”

Baada ya maneno hayo, Kamati imejiridhisha kumkuta hatiani Haji Manara na kumfungia miaka miwili kutojihusisha na soka ndani na nje ya nchi na kumtodha faini ya Sh20 milioni adhabu ambayo inaanza rasmi kuanzia leo Julai 21 mwaka 2022 japo anauwezo wa kukata rufaa.

Post a Comment

0 Comments