Ticker

6/recent/ticker-posts

Sterling Rasmi Atua Chelsea

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

MSHAMBULIAJI wa kimataifa, Raheem Sterling, 27, amejiunga na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano utakaomalizika 2027.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Uingereza, amekuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa rasmi na klabu hiyo tangu ujio wa mmiliki mpya Todd Boehly, na atajiunga na kikosi cha Thomas Tuchel nchini Amerika kwa mazoezi.


Chelsea imepiga kambi nchini Amerika ambapo imepangiwa kupimana nguvu na Club America, Charlotte FC na Arsenal.

Kulingana na mkataba huo ambao una kipengele cha kumkubalia aendelee, Chelsea imeanza kwa kulipa Manchester City Sh6.3 bilioni kama malipo ya kwanza, na baadaye itoe Sh1.4 bilioni, iwapo nyota huyo atang’ara na kuendelea kuwa katika kikosi cha kwanza pale Stamford Bridge.

Kulingana na ripoti za hivi punde, Sterling alifanyiwa vipimo vya kimatibabu jijijini hapa, na kusaini mkataba wake mara tu zoezi hilo lilipokamilika.

Fabrizio Romano ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uhamiaji wa wachezaji barani Ulaya, alidokeza kwamba Raheem Sterling amejiunga rasmi na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano.

Chelsea wanaimarisha kikosi chao ili kufikia kiwango cha Manchester City ambao wamekuwa wakiwika ligini, misimu ya karibuni.

Muda mfupi baada ya kumnasa Sterling, kumetokea uvumi mwingine kwamba mlinzi hodari Kalidou Koulibaly pia anakaribia kunaswa na Tuchel, kujaza nafasi ya Antonio Rudiger aliyehamia Real Madrid.

Koulibaly amekuwa kwenye rada ya Chelsea kwa muda mrefu, na sasa raia huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 31 huenda akapewa Sh4.7 bilioni.

Mmiliki wa Napoli Aurelio De Laurentiis amekuwa akipandisha bei ya nyota huyo, hasa tangu timu ya taifa ya Senegal inyakuwe ubingwa wa Mataifa ya Afrika.

Lakini, akiwa amebakisha mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa sasa, Laurentiis amekubali kumuachilia ajiunge na Chelsea kwa mkataba wa kudumu.

Koulibaly mwenyewe amesema mazungumzo kuhusu mkataba huo yamepiga hatua kubwa na kuongeza kwamba yuko tayari kabisa kuhamia Stamford Bridge.

Dili hilo likifaulu, Koulibaly atakuwa akipokea Sh1.2 bilioni kwa mwaka (karibu Sh88.6 millioni kwa mwezi na Sh25.3 milioni kwa wiki)

Post a Comment

0 Comments