Ticker

6/recent/ticker-posts

Namungo FC: Shiza Kichuya Afunguka Usajili Simba

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Namungo FC: Shiza Kichuya Afunguka Usajili Simba


WINGA wa Namungo FC, Shiza Kichuya amesema mkataba wake na timu hiyo ya mkoani Lindi unatarajiwa kumalizika mwezi huu, lakini anaweza kubaki klabuni hapo endapo watafikia makubaliano na mabosi wake.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri msimu uliomalizika, Kichuya ametajwa kutakiwa na timu yake ya Simba huku Namungo bado ikiwa pia inahitaji huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.

Kichuya alisema atakuwa tayari kumwaga wino kwa timu ambayo itakubali kumpatia kiasi cha fedha anachohitaji kwa sababu mchezo wa mpira wa miguu ndio kazi yake.

Hata hivyo Kichuya ameweka wazi hakuna kiongozi yoyote ya Simba aliyemfuata rasmi kwa ajili ya mazungumzo ya kusaini mkataba zaidi ya kuzisikia taarifa hizo kwenye baadhi ya vyombo vya habari.

"Siku zote wachezaji wanaweza kucheza popote pale kwa ajili ya kutafuta maisha na si vinginevyo. Mkataba wangu upo mbioni kumalizika mwezi huu, kama Namungo watahitaji huduma yangu na wakifika dau linalotaka basi nitasalia. Sisi wachezaji tunacheza kwa ajili ya kutafuta pesa ili tusaidie familia zetu," alisema Kichuya.

Winga huyo alisema bado ana kiwango kizuri na anaamini anaweza kutoa mchango mkubwa kwa timu itakayomsajili.

"Mashabiki wananipigia na kunikaribisha, utasikia 'karibu nyumbani', sasa mimi mtu akiniambia hivyo namuuliza anapoishi, namwambia unaishi wapi nije? Msimu ukiisha nitakuja kukutembelea, ananijibu 'simaanishi hivyo', kumbe wao wanaona kwenye vyombo vya habari kuwa eti nimesajiliwa Simba, ukweli sijawahi kupokea simu ya kiongozi yoyote wa klabu hiyo. Labda, inawezekana wakaja baadaye." Kichuya aliongeza.

Winga huyo aliichezea Simba mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar hadi 2018, kabla ya kwenda Pharco ya Misri halafu akarejea tena Simba kwa muda mfupi kabla ya kutimkia Namungo na amekuwa na kiwango bora msimu uliomalizika.

Post a Comment

0 Comments