Ticker

6/recent/ticker-posts

Serge Gnabry Akataa Mamilioni Ya Bayern Munich

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

 Serge Gnabry Akataa Mamilioni Ya Bayern Munich

KLABU ya Manchester City, Imeungana na watani wao Manchester United katika vita vya kuwania saini ya fowadi mahiri wa Bayern Munich, Serge Gnabry.

Nyota huyo wa zamani wa Arsenal anaongoza orodha ya washambuliaji wanaopiganiwa na kocha Pep Guardiola katika juhudi za kujaza pengo la mshambuliaji Raheem Sterling anaye  takiwa na Chelsea.

Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea wako radhi kuweka mezani kima cha Sh5.2 bilioni ili kujinasia maarifa ya Sterling au Cristiano Ronaldo wa Man-United kujaza pengo la Romelu Lukaku aliyerejea kwa mkopo Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Ingawa Bayern wana hamu ya kumdumisha Gnabry ambaye amekuwanao tangu 2017, mshambuliaji  huyo anayemezewa pia na Arsenal, amekataa kutia saini mkataba mpya kwa ofa ya Sh33 milioni kwa wiki uwanjani Allianz Arena.

Kwa kuwa Gnabry, 26, amesalia na miezi 12 pekee katika mkataba wake wa sasa na Bayern, miamba hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) watakuwa radhi kumtia mnadani badala ya kumwachilia atafute hifadhi mpya kwingineko bila ada yoyote muhula ujao.

Man-City wana kiu ya kusajili fowadi atakayeshirikiana na sajili wapya Erling Haaland na Julian Alvarez katika safu yao ya mbele baada ya Gabriel Jesus kuyoyomea Emirates kuvalia jezi za Arsenal. Man-United kwa upande wao wanasaka mshambuliaji atakayechukua mahali pa Cristiano Ronaldo ambaye ametaka waajiri wake wamruhusu aondoke ugani Old Trafford.

Zaidi ya Gnabry, kocha Erik ten Hag anayelenga kusuka upya kikosi chake cha Man-United, tayari amemsajili beki Tyrell Malacia kutoka Feyenoord ya Uholanzi kwa Sh2.3 bilioni. Mkufunzi huyo anahemea pia huduma za kiungo mvamizi wa Barcelona, Frenkie de Jong, na wanasoka wawili wa Ajax – Antony Matheus dos Santos na Lisandro Martinez anayehusishwa pia na Arsenal.

Man-City wanapania pia kusajili beki Marc Cucurella wa Brighton kwa Sh6.7 bilioni ili kumpiga jeki Kalvin Phillips aliyetokea Leeds United kwa Sh6 bilioni mwezi uliopita kujaza nafasi ya nahodha Fernandinho Luiz Roza aliyerejea Brazil kuchezea Athletico Paranaense.

Kufikia sasa, Man-City wamemwaga sokoni kima cha Sh16 bilioni kwa ajili ya wanasoka wapya huku wakipata Sh40 bilioni baada ya kuuza masogora kadhaa, akiwemo Ferran Torres aliyejiunga na Barcelona kwa Sh8 bilioni mnamo Januari 2022.

Post a Comment

0 Comments