Ticker

6/recent/ticker-posts

Rekodi za CAF zambeba kocha mpya Simba

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Rekodi za CAF zambeba kocha mpya Simba

 


JUZI usiku Simba ilimtambulisha Zoran Manojlovic Maki mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno kama kocha wake mkuu akichukua mikoba ya Mhispania Pablo Franco iliyempa mkono wa kwaheri baada ya kushindwa kufikia malengo.

Simba imemteua Maki kati ya makocha zaidi ya 100 waliotuma wasifu wao na kuomba kazi ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wake Barbara Gonzalez, huku ikielezwa rekodi tamu alizonazo kwenye michuano ya CAF ndio iliyombeba.

Maki mwenye umri wa miaka 59 ni mbobezi wa soka la Afrika, kwani amefundisha klabu mbali mbali ndani ya bara hili na kuzipa mafanikio tofauti kubwa zaidi ikiwa kuifikisha Primero de Agosto ya Angola katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018. Na kikubwa Simba wanacholenga msimu ujao ni nusufainali ya Afrika. “Huwezi kuongozwa na mtu ambaye hajui njia utapotea, Maki anaijua njia ya nusufainali ya Afrika kwavile alishaipita,”alidokeza kiongozi mmoja wa usajili wa Simba.

Maisha yake ndani ya soka la Afrika yalianzia nchini Angola ndani ya Primero (2010-2011) kisha kujiunga na Kabuscorp mwaka 2012 ya hukohuko akiwa kama kocha msaidizi na hapo alishinda kombe la Ligi Kuu mwaka 2014 likiwa pekee katika historia ya timu hiyo sambamba na Kombe la Super Cup.


REKODI ZA CAF

Mwaka 2017 Maki alijiunga na Primiero de Agosto ya Angola na kuinoa hadi mwaka 2019 huku akiifikisha nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, rekodi ambayo ni kubwa zaidi kwakwe kwenye soka la Afrika. Alifanya hivyo msimu wa 2018.

Katika nusu fainali hiyo Primiero ilikutana na Esperance de Tunis ya Tunisia na kushinda mechi ya kwanza 1-0 lakini ugenini ilifungwa 4-2 na kutolewa kwa wastani wa mabao 4-3 na msimu huo Esperance ilibeba ubingwa kwa kuifuna Al Ahly ya Misri katika fainali ikipoteza mechi ya kwanza ugenini kwa kuchapwa 3-1 lakini ikipindua meza nyumbani kwa ushindi wa 3-0 na matokeo ya jumla kuwa 4-3. Pia Maki aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Angola Primero mwaka 2019 kabla ya kuondoka na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco.

Akiwa Wydad msimu wake wa kwanza 2019/2020 aliifikisha kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa na kurudi kujipanga upya na mwaka 2021 aliifikisha robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Baada ya hapo alijiunga na Al Hilal ya Sudan ambako hakufanya maajabu makubwa na kukaa muda mfupi kisha kujiunga na wababe CR Belouzidad ya Algeria ambako alishinda Ligi Kuu nchini humo mwaka 2021.

Mafanikio hayo yalimfanya apate fursa ya kuinoa Al-Tai ya Saudi Arabia mwaka jana, lakini hakudumu ndani ya timu hiyo kutokana na mwenendo mbovu na kukaa bila timu hadi sasa alipojiunga na Simba.

Timu nyingine alizowahi kuzinoa ni Trofense, (2000-2001), Vila Real (2006-2007) na Alcains 2009 zote za Ureno.


FALSAFA ZAKE

Maki mwenye Leseni ya UEFA Pro anapendelea sana soka la kujilinda na kushambulia kwa kasi huku akipendelea kutumia mifumo ya 4-4-2, 5-3,2 na 4,3,3 katika mechi zake nyingi.

Huenda Simba ikabadilika kiuchezaji kutoka kwenye soka la pasi fupi fupi na kwenda kwenye pasi ndefu za mbali na kuwa na kasi katika kutengeneza nafasi.

Wachezaji wenye kasi kwa kocha huyu wanapata nafasi kubwa sambamba na viungo wa ulinzi hivyo huenda kina Jonas Mkude na Sadio Kanoute pamoja na Kina Kibu Denis, Peter Banda, Pape Sakho na Moses Phiri wenye spidi wakawa na nafasi kubwa ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao.

Miongoni mwa maelekezo Simba iliyompa Maki ni jukumu la kuifanya Simba kurudi kwenye makali yake na ubora ikiwemo kutwaa Kombe la Ligi Kuu Bara, ASFC, Mapinduzi na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza  Ofisa Habari wa Simba Ahmed Ally amemuelezea kocha huyo kuwa na ubora mkubwa hivyo wanaimani ataifikisha Simba katika malengo.

“Tumemuamini, historia yake ndani ya soka la Afrika ni kubwa na tunaamini kwa ushirikiano wa kila mtu ndani ya Simba tutafika malengo na kocha huyu,” alisema Ally.

Msimu huu Simba iliishia kwenye robo fainali ya CAF na kumaliza ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania bara, rekodi ambayo haitaki ijirudie msimu ujao.

“Tuna matarajio makubwa na Zoran, klabu imempa malengo yake ambayo ni kufika nusu fainali ya CAF na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao,” alisema Ahmed.

Kuhusu kumpa mkataba wa mwaka mmoja kocha huyo, Ahmed alisema hayo ni masuala ya ndani na makubaliano ya pande zote mbili hivyo hawezi kuyazungumzia kwa undani.

“Kama klabu tuna imani na kocha Zoran, ni kocha mwenye rekodi na mzoefu kwenye soka la Afrika, hivyo tunatarajia atatufikisha na kutuvusha katika malengo ya klabu msimu ujao.

Alisema kocha huyo atashiriki kwenye mapendekezo ya usajili msimu huu wa dirisha kubwa ambalo timu hiyo itaongeza nyota wapya wa kigeni watano kwa mujibu wa Ahmed.

Post a Comment

0 Comments