Ticker

6/recent/ticker-posts

Msuva Azibwaga Simba Na Yanga

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Msuva Azibwaga Simba Na Yanga

ILIKUWA safari ya kicheko kwa Saimon Msuva kwa mara ya kwanza, alipopata ofa ya kucheza Difaa El Jadida ya Morocco msimu wa 2017 hadi 2020 na baadae kutimkia kwa mabingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu, Wydad Casablanca alikosajiliwa mwaka 2020.

Msuva wakati anakwenda kuyaanza maisha ya soka Morocco alikuwa ametokea klabu ya Yanga alipomaliza msimu wa 2016/17 akiwa kinara wa mabao 14 sawa na Abrahaman Mussa wa Ruvu Shooting.

Hata hivyo Novemba mwaka jana, Msuva alingia katika mgogoro na Wydad Casablanca hivyo kuamua kupelekea malalamiko Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) akidai klabu hiyo kushindwa kumlipa baadhi ya stahiki zake kinyume na makubaliano ya mkataba.

Julai 11, Fifa iliwapa siku 15 klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco kumlipa Msuva dola za kimarekani 700,000 (zaidi ya Sh1.6 bilioni) baada ya kushinda kesi dhidi ya klabu hiyo.

Pamoja na mafanikio aliyoyapata Morocco ya kupandisha thamani yake ya biashara kisoka, Msuva anafunguka mambo mengi yaliyosababisha kukaa nje ya uwanja kwa miezi saba na namna asivyopenda hata kuizungumzia Wydad Casablanca kwa sasa.

Kesi ilivyompa mawazo

Msuva anaanza kwa kushusha pumzi na kusema jinsi kesi ilivyokuwa inamnyima usingizi kwani muda mwingi alikuwa akiwazia jambo hilo litakuaje.

“Unajua unapokuwa na kesi mara nyingi unakuwa na shauku ya kutaka kujua lini inasomwa kesi yako japo FIFA walitoa taarifa kwamba kesi yangu ingesomwa mwezi wa tano ila hawakutaja tarehe, lakini pia wakabadilisha wakasema itasomwa mwezi wa saba.

“Nikashauriana na wanasheria wangu na kuwaambia kuwa nahitaji kurejea uwanjani kucheza ndipo baadae ikaja taarifa kuwa kesi itasomwa kati ya Julai 5, 6 au 7 ila mwisho wa siku ni kama wakatushangaza kwani kesi ilisomwa muda mwingine ambao hatukutarajia, “anasema Msuva na kuongeza;

“Nimepokea uamuzi huu kwa furaha kwani nilikaa muda mrefu nje ya uwanja na ukizingatia kama mchezaji wa timu ya Taifa na watanzania wanamuamini na kumkubali na leo hii anakuwa hayupo kwenye kazi ni kitu ambacho kinawia ugumu

“Nilikuwa sio Simon mimi, watu wengi walikuwa hawajui niliyokuwa nayapitia, nimeishi katika mazingira fulani magumu ila nashukuru watu wangu wa karibu waliokuwa wananipa ushauri kunihimiza niendelee kufanya mazoezi na kujifunza.

Msuva anasema anaishukuru sana familia yake ambayo ilikuwa ikifunga kwa maombi kuhakikisha jambo hilo linamalizika salama.

“Ujue sio mimi tu ila mfanyakazi yoyote aliyezoea kuwa kazini halafu anakuwa hayupo takribani miezi mitano mpaka saba lazima imuwie ugumu kwenye maisha, kwa upande wangu niliweza kukaa na familia yangu karibu na kujitahidi kumuomba Mungu ili suala liweze kuisha.

“Hili jambo lilikuwa kama kucheza kamari ingawa nilikuwa na nafasi ya kushinda lakini ulikuwa huwezi jua kwani waarabu wana mbinu nyingi na wangeweza kufanya chochote bila sisi kujua halafu ikaonekana kesi iko upande wao, kwa hiyo nashukuru Mungu tumepata majibu mazuri lakini nilikuwa naomba leo au kesho kesi imalizike.

Kesi ilipoanzia

Msuva anasema wala hakuwa na shida na kocha wala wachezaji wenzake wa Wydad Casablanca lakini tatizo kubwa lilikuwa kwa rais wa klabu hiyo.

“Unajua tangu nifike Morocco nilikuwa freshi tu nikianzia katika klabu ya Difaa El Jadida. Licha ya kwamba ilinipa shida kidogo kwenye lugha na chakula lakini nilishazoea hivyo hata nilivyohamia Wydad Casablanca hakukuwa na kitu kigeni kwangu.

“Ugumu ndani ya klabu ya Wydad ulikuja baada ya kuanza kudai hela yangu, lakini wachezaji wenzangu na kocha tulikuwa tunaelewana sana ila tatizo liikuwa kwa rais wa timu

Msuva anasema hawakuwa na maelewano mazuri na rais wa klabu hiyo baada ya kuwa mgumu kumlipa fedha zake licha ya kwamba kulikuwa na makubaliano ya kimkataba.

“Jamaa ana dharau sana kwani haiwezekani mfanyakazi wako tena sio raia wa Morocco lakini unamchukulia kawaida licha ya kwamba nilikuwa nafanya kazi ikiwemo kufunga na naanza kikosi cha kwanza.

“Baada ya kuona nimedai na akawa mgumu, nikafuata sheria zote ikiwemo kuandika barua ya kwanza, ya pili na ya tatu ambayo niliwapa siku 15 kwa kuwaambia kuwa kama wasingenilipa ningevunja mkataba na ndio nilivyofanya ,”alisema Msuva na kuongeza.

“Nilisaini mkataba wa miaka minne unaomalizika mwaka 2024 na katika kipengele cha makubalino yangu kwenye usajili walitakia wanilipe sehemu ya pesa kila mwaka kwa awamu tatu (Package).

“Nilitakiwa kulipwa kwa miezi miwili ya mwanzo (Januari na Februari), mwezi wa nne na tano na mwezi wa saba na nane ambapo ligi inapomalizika lakini wao wakanipa kwa miezi miwili ya mwanzo tu na iliyofuata hawakunipa chochote lakini cha kushangaza rais akawa anatangaza kuwa ameshanipa hela na wakati sio kweli na akagushi hadi saini kuwa nimechukua hela simdai chochote na nafikiri hivyo vitu vimechangia kumshinda katika kesi na yeye amefungiwa nafikiri kwa miaka miwili,” anasema Msuva.

Alipokeaje humuku ya FIFA

Msuva anasema hakuna siku aliyofurahi kama alivyopokea taarifa ya kushinda kesi hiyo licha ya kwamba ni kama alipata ganzi kabla ya kufurahi baadae

“Kwanza kuna mtu huwa ananisimamia mimi ambaye ni mtanzania na aliniunganisha na wanasheria wawili kutoka nje ya nchi ambao ndio walikuwa wanasimami kesi yangu.

“Sasa huwa tuna kundi letu la ‘Whatsapp’, hukumu ilipotoka kwanza alinipigia yule msimamizi wangu mtanzania nikajua masihara tu kwa sababu tumeshazoea kutaniana lakini akaniamnia ingia kwenye kundi uone ndio nikakuta vile vithibitisho vyote kutoka FIFA kuwa nimeshinda kesi. Nilifurahi sana kiukweli na kuiambia familia yangu ambayo nao walifurahi kwani walikuwa hawajui, na tukashukuru Mungu kwa pamoja kwa kujibu maombi yetu , “anasema Msuva.

Awachukia Wydad

Msuva anasema licha ya kwamba hakuwa na ugomvi na wachezaji wala kocha wa klabu yake lakini alijikuta tu anaichukia timu hiyo hadi sasa.

“Nilikuwa sipendi kuwaangalia Waydad wala kuwafutilia kwa chochote walichokua wakikifanya, kwani ilitokea tu kumchukia rais na timu japo sikuwa na ugomvi na kocha wala mchezaji yoyote na kocha alikuwa akinipenda sana.

“Nilijua kuwa watachukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwani nilikua naona matamanio yao tangu mimi nipo ndani ya timu hiyo na kama wangeishia nusu fainali ningeshangaa,” anasema Msuva.

Maneno yalimuumiza

Baada ya Msuva kurejea Tanzania huku ikidaiwa amegoma kuendelea kuichezea Wydad Casablanca, wengi walishangaa uamuzi wake huku wengine wakimtolea maneno makali kuwa ndio kawaida ya wachezaji wa kitanzania kutokuwa wavumilivu wanapokwenda kucheza soka nje ya nchi.

Kumbe Msuva alikuwa akisikia maneno hayo na hata kuyasoma kwenye mitandao ya kijamii lakini alimwachia Mungu.

“Maneno yalikuwa mengi na yaliniumiza sana sana sana hasa ya kwamba huyu hana klabu lakini anaitwa timu ya Taifa. Ilikuwa inawapa wakati mgumu pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na makocha wa Taifa Stars kwa sababu wao ndio wanachangua mchezaji gani anafaa kuwepo kwa muda huo.

“Nilikuwa naumia kusikia maneno ya kebehi na mengine nayaona kwenye mitandao ya kijamii lakini nilijipa moyo na niliyachukulia maneno hayo kama darasa kwangu, kwa wachezaji wengine na kwa watanzania kwa jumla kwani kukaa kwangu muda mrefu nje ya uwanja Mungu ameonyesha kitu fulani kwangu na watu wengine kwamba katika maisha wakati mwingine panahitajika umuvilivu, “anasema Msuva na kuongeza;

“Unaweza ukahitaji kitu kwa muda huo lakini Mungu asikupe kwa muda huo huo na akakupa kwa muda mwingine kabisa ambapo wewe hujategemea

“Mimi sikutegemea kama kesi itamalizika sasa kwani nilihisi itachukua hata mwaka kwani majibu waliyokuwa wananipa wanasheria wangu walikuwa akijibu kuwa Kesi Fifa zipo nyingi nashukuru Mungu kesi imekwisha na tuangalie mengine.

Aikataa Bongo

Msuva anasema matamanio yake kwa sasa ni kucheza ska nje ya nchi ili kupata pesa nyingi kwa sababu familia yote inamuangalia yeye.

“Kwanza sitaki kusikia habari za klabu bingwa Afrika kwani kama nimeshindwa kuchukua kombe au kuvaa medali nikiwa Wydad siwezi kuvaa sehemu nyingine yoyote tena.

“Malengo yangu hivi sasa ni kupata pesa nyingi ya mpira, nahitaji kufaidika na kuna nchi ambazo nimezilenga kama Qatar, Saudi Arabia, Dubai, hizi ndio nataka kucheza hata kama watu wataongea kuwa huyu hana akili kwa nini kaenda huko bora angeenda Ulaya, sijali wala nini kila mtu na maisha yake, “anasema Msuva na kuongeza; “Kama itatokea nafasi ya kwenda Ulaya nitakwenda ila nchi hizo zilizozitaja ndio kipaumbele changu cha kwanza kwani naamini nitapata hela na mpira nitacheza

“Ujue Ulaya inawezekana hela ipo lakini sio hela ninayoitaka mimi lakini pia ukizingatia na pasipoti yangu inavyosema. Ujue mimi sina miaka 20, Ulaya inahitaji muda, kwa sasa kidogo umri umesogea hivyo lazima niwe na malengo nipate sehemu ambayo itakidhi mahitaji yangu maisha yangu kwani mwisho wa siku watu wataangalia maisha yako yakoje na hawatangalia historia yako kwamba umecheza Ulaya au wapi, ingawa hitoria ni nzuri kwenye maisha ila historia bila hela si chochote, “anasema Msuva.

Yanga, Simba vipi?

Msuva anasema klabu zote mbili zilihitaji huduma yake ikiwemo na Azam lakini ameshawaambia kuwa kwa sasa hana malengo ya kucheza soka Tanzania. “Labda siku zijazo naweza kurudi kucheza soka Tanzania na kumalizia soka langu kwenye nchi yangu lakini kwa sasa chaguo langu la kwanza hadi la tatu ni kucheza nje ya nchi”.

“Ikitokea nikacheza Bongo kwa sasa labda machaguo yangu yote matatu yafeli lakini nina ofa saba hadi nane, za Ulaya mbili na tano za nchi za Uarabauni ila siwezi kutaja klabu hadi hapo dili litakapokamilika ndio nitataja naenda wapi.”

Post a Comment

0 Comments