Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwa Yanga Hii...Simba Mtasubiri Sana

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Kwa Yanga Hii...Simba Mtasubiri Sana

JUZI Jumamosi klabu ya Yanga imefanya uchaguzi wa viongozi wapya. Ndio uchaguzi wa kwanza baada ya kupita kwa katiba mpya inayohalalisha mfumo mpya wa mabadiliko.

Nawatakia kheri viongozi wote waliochaguliwa. Wana kazi kubwa sasa ya kwenda kusimamia mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ya klabu hiyo. Kila mtu alisubiri kwa miaka Yanga kuwa na mfumo mpya, lakini sasa inawezekana kubadilika.


Unadhani ni mara ya kwanza Yanga kufanya mabadiliko haya? Hapana. Wamewahi kufanya huko miaka ya nyuma lakini haikuzaa matunda. Walifanya wakati ule wa Abbas Tarimba akiwa Mwenyekiti.


Yanga ikatengeneza katiba mpya kama sasa. Katika mfumo wa wakati huo wakataka moja iwe Yanga kampuni na nyingine ya Wanachama. Hata hivyo mchakato huu haukuzaa matunda.


Wanayanga wengi wakaupinga. Hasa wazee wa Yanga. Wakati ule Yusuf Manji akiwa mfadhili akajaribu kuleta Mtendaji Mkuu kutoka Kenya kuja kusimamia mchakato huo. Wazee wakamkataa.


Mchakato ukabaki kwenye Katiba tu, lakini haukuzaa matunda. Yanga ikaendelea kuendeshwa kizamani. Ikabaki kuwa vile vile.


Lakini kwa kuwa baadaye Manji alijitokeza na kusimamia mambo yote, haikuonekana kama ni tatizo. Manji aliifanya Yanga kuwa imara sana ndani ya nchi.


Akavunja ufalme wote wa Simba. Akasajili wachezaji wakubwa. Akalipa kambi ya timu na mishahara. Yanga ikawa kubwa sana. Ikaogopwa ndani na nje ya nchi.


Lakini haya yote Manji alifanya kwa utashi wake. Alifanya kwa mapenzi yake. Kwa kuwa alitoa gharama zote, hakuna aliyewahi kulalamika. Mambo yalikwenda vizuri.


Awali alianza kama mfadhili na baadaye akawa Mwenyekiti. Kwanini Manji na utajiri wake aliamua kuwa Mwenyekiti wa Yanga? Ni kwa sababu alikuwa anatoa fedha nyingi. Alitaka kuwa na mamlaka na fedha anazotoa. Alitaka kuona kwa karibu fedha zinatumikaje.


Katika hili alifanikiwa. Wakati Yanga ikiwa chini ya Manji nidhamu ilikuwa kubwa. Maendeleo Uwanjani yalionekana. Alileta makocha wakubwa na kuwalipa vizuri. Alifanya kila kitu.


Lakini pamoja na yote hakuweka nguvu kusimamia yale mabadiliko ya Katiba Mpya. Aliacha mfumo wa zamani uendelee kufanya kazi. Mfumo ambao ulimtegemea yeye.


Akaja na mfumo mpya wa kutaka kuikodi timu kwa miaka 10. Akasema atawapa klabu asilimia 25 ya faida itakayopatikana. Wamuachie gharama na kila kitu juu yake Wasubiri faida.


Yanga wakagoma. Marehemu Mzee Yahya Akilimali akasema Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya pilau. Jambo likakwama.


Nini kilitokea baada ya Manji kuondoka? Yanga ilianguka kama kinyonga anayejifungua. Ikawa timu masikini kweli kweli. Haikuvutia hata kidogo. Yaani ikawa kama mwanaume mwenye sura mbaya halafu hana pesa. Mwanamke gani atampenda?


Hata hivyo, sasa Yanga imejaribu mfumo mpya tena. Imetengeneza Katiba madhubuti na kuweka mfumo mpya wa uendeshaji. Pengine sasa unaweza kufanya kazi. Kwa nini? Subiri nitakwambia.


Kwanza, kila mtu anakubali kuwa nyakati hizi mpira unahitaji fedha. Tena sio fedha kidogo. Wakati ule wanaweka mfumo mpya mwaka 2007 mchezaji ghali aliuzwa dola 20,000 (Sh46 milioni). Sasa mchezaji wa kawaida tu anauzwa Dola 100,000 (Sh230 milioni. Ni mara nane zaidi.


Fedha hizo zinatoka wapi? Usajili pekee tu unaweza kugharimu zaidi ya Sh1.5 bilioni. Hiyo ni kwa msimu mmoja tu. Vipi kuhusu mambo mengine? Ni gharama kubwa.


Nyakati za sasa kuendesha timu kama Yanga na ifanye vizuri ndani na kimataifa unahitaji sio chini ya Sh8 bilioni kwa msimu. Nani anatoa fedha hizo? Ni swali ambalo halina jibu.


Majibu ni mfumo mpya wa uendeshaji. Wanatakiwa wawekezaji wa nguvu. Wanatakiwa viongozi imara wa kusimamia mabadiliko haya. Hiki ndicho Yanga inafanya sasa.


GSM baada ya kutoa fedha kwa mwaka mmoja pale Yanga aliona ulazima wa mfumo huu mpya. Ndio maana akakubali kulipa fedha kuratibu mchakato mzima.


Baada ya hapo anahitaji mtu ambaye anaweza kusimamia mabadiliko haya yakamilike. Hapa ndio pagumu zaidi. Mabadiliko kukamilika ni jambo linalohitaji nia na usimamizi wa dhati.


Ndio maana pale Simba mpaka sasa haifahamiki kama mfumo mpya umekamilika ama la.


Mambo hayaeleweki kabisa. Kwa nini? Kwa sababu hakuna usimamizi wa kweli wa mchakato.


Hii ndio sababu GSM ametaka kuwa ma watu wake kwenye uongozi wa sasa kuhakikisha mambo yanakamilika.


Viongozi wapya wana kazi kubwa ya kuhakikisha wawekezaji wanapatikana na mfumo mpya unafanya kazi.


Wakifanikiwa tutaona Yanga ikienda kuwa klabu kubwa Afrika. Yanga ikiwa imara zaidi nchini. Vinginevyo watakuwa wamepoteza muda tu.


Nawatakia kheri viongozi wapya wa Yanga katika kusimamia mchakato huu wa mabadiliko. Wajifunze ambapo Simba walikwama nao wasonge mbele zaidi.


Katika jambo hilo hakuhitajiki siasa. Yanahitajika maono na usimamizi mkubwa. Wakienda kwa siasa watamaliza miaka yao minne wakiwa hawana lolote la kujivunia.

Post a Comment

0 Comments