Ticker

6/recent/ticker-posts

Kocha Simba aleta mifumo mitatu

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KAMBI ya Simba imezidi kunoga baada ya beki Mohamed Ouattara aliyetambulishwa juzi kutoka Al Hilal ya Sudan kuanza tizi na wenzake huku akionekana wamoto, lakini utamu ni Kocha Zoran Maki kuitambulisha falsafa yake ikiwa na mifumo mitatu matata kikosini.

Ouattara raia kutoka Burkina Faso ameungana na wenzake kambini mjini Ismailia na kuzidi kuinogesha kambi hiyo, kwani anakuwa mchezaji wa sita kati ya wanane waliosajiliwa dirisha la usajili linaloendelea kuwa wazi hadi Agosti 31, baada ya Nassor Kapama, Habib Kyombo, Vicent Akpan, Moses Phiri na Augustine Okrah

Wachezaji ambao bado hawajatambulishwa ni Nelson Okwa na Cesar Manzoki ambaye hata hivyo, klabu yake ya Vipers ya Uganda imeweka ngumu kumwachia, hivyo huenda akasajiliwa kupitia dirisha dogo la Desemba mwaka huu.

Beki huyo mwili jumba na mwenye urefu wa mita 1.85 ambayo ni sawa na futi 6.1, ametua Msimbazi ili kuziba nafasi Pascal Wawa aliyemaliza mkataba wake na klabu hiyo na kudakwa juu kwa juu na Singida Big Stars.


MIFUMO MITATU

Wakati Ouattara akianza mambo Simba, kocha wa timu hiyo Zoran Maki ameendelea kukisuka kikosi chake kwa kuwapigisha tizi mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni.

Katika mazoezi hayo Zoran ameyagawanya sehemu mbili, ikiwemo kufanya yale ya gym na uwanjani ila kuna nyakati hufanya ya mbinu huku wachezaji wakitumia mipira.

Kocha huyo Mreno mwenye asili ya Serbia amekuwa akijaribu mifumo mitatu tofauti na huenda mmoja kati ya hiyo au yote akaitumia katika mechi ya kwanza ya kimashindano ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Agosti 13, itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mechi hiyo Simba pia itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa katika kilele cha Tamasha la Simba Day Agosti 8 kisha ndipo itavaana na Yanga.

Mfumo wa kwanza Zoran alionekana kuufanyia kazi ni ule wa (4-2-3-1), ambao Simba ilimaliza nao msimu ikiwa chini ya makocha Pablo Franco na Selemani Matola. Mfumo huo wa 4-2-3-1, kwa maana ya mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na straika mmoja Zoran alianza nao katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ismailia uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, kabla ya kuibadilisha kwenye kipindi cha pili.

Mfumo mwingine Zoran alitumia ilikuwa na (4-3-3), uliokuwa na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu Pape Sakho, Augustine Okrah na Chriss Mugalu ulioonekana kufanya vizuri wakicheza kwa maelewano makubwa.

Mfumo wa mwisho Zoran alitumia (4-1-3-2) kwa maana ya mabeki wanne, kiungo mkabaji mmoja, viungo washambuliaji watatu na washambuliaji asilia wawili.

Zoran katika mfumo huu watatu alikuwa na dhumuni la kushambulia zaidi ndio maana aliweka kiungo mmoja wa ukabaji na wachezaji wengine watano waliokuwa juu yake wana asilia na ubora wa kushambulia zaidi.

Simba mara ya mwisho kutumia mfumo huo na kawapa faida ilikuwa Januari 10, 2021 katika mechi ya pili Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji iliyowapa ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani dakika ya 71 na Meddie Kagere enzi za kocha Didier Gomes kabla ya kutimuliwa na kuletwa Pablo.

Kabla ya hapo mfumo huo ulikuwa ukitumika zaidi enzi za Kocha Patrick Aussems na kwenye eneo la washambuliaji wawili alikuwa akiwaweka, Kagere na John Bocco.

Akihojiwa akiwa nchini Misri, Zoran alisema wanaendelea na maandalizi ya kila aina kulingana na ratiba ya siku ilivyo ili kuhakikisha wachezaji wote kutumia vizuri kujiandaa vizuri miili yao na kuwa tayari kwa ushindani. Zoran alisema wanafanya mazoezi ya nguvu pamoja na hiyo mifumo ikiwemo kujaribu katika mechi za kirafiki ili wachezaji kuanza kuzoea mapema vitu vya kufanya kabla ya mechi za kimashindano kuanza.

“Naimani haya mazoezi yote ambayo tunayafanya huku katika nyakati tofauti tutakwenda kuyatumia katika michezo ya kimashindano na lengo kubwa kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye mashindano yote msimu ujao,” alisema Zoran aliyewahi kung’ara katika michuani ya CAF akiwa na Premiero do Agosto ya Angola, Wydad Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan.

Post a Comment

0 Comments