Ticker

6/recent/ticker-posts

Hivi Ndivyo Yanga Walivyoikamata Saini Ya Stephane Aziz Ki

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Hivi Ndivyo Yanga Walivyoikamata Saini Ya Stephane Aziz Ki

YANGA imemaliza utata kuhusu usajili wa nyota wake mpya kutoka Burkina Faso, Stephane Aziz Ki kutoka klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast baada ya kumshusha kimafia usiku wa kuamkia juzi, lakini kuna filamu moja ya kibabe ilifanyika katika ujio wa staa huyo.

Baada ya “anakuja-haji” kutawala kwa muda mrefu, Aziz Ki alitua nchini akitumia Ndege ya Shirika la Ethiopia ambayo iligusa ardhi ya Tanzania saa 9:10 usiku.


ULINZI MKALI UWANJANI

Wakati Yanga ikimshusha KI, kuna umafia mkubwa ulifanyika kuhakikisha hakuna mtu anabahatika kupata hata picha yake wakilenga kutaka kushtua kwa utambulisho wa mshambuliaji huyo uliotarajiwa kufanyika usiku .


Ndani ya uwanja huo mara baada ya ndege kutua kisha abiria kuanza kutoka KI alikuta tayari watu maalum wakimsubiri ambao walizuia kupiga naye hata picha ya simu kisha kupelekwa sehemu maalum ambayo alikamilisha taratibu za kuingia nchini kwa mujibu wa sheria.


“Kuna watu walitaka kupiga naye picha kama wanavyokuja wachezaji au makocha, lakini wakati abiria wanaanza kutoka tu kuna watu wawili hatuwajui walikuwa wanamsubiri mulemule ndani, wakamfuata na kutuzuia kufanya lolote,” alisema mmoja wa maafisa wa ndani ya uwanja huo na kuongeza;


“Alikuwa amefuatana na huyo mwanamama nafikiri ndio mama yake, KI alikuwa amevaa kaptula na shati lenye vyumbavyumba ya rangi nyeupe na nyeusi.


Mara baada ya kukamilisha taratibu hizo mshambuliaji huyo wa zamani wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast alitolewa kupitia mlango wa VVIP kimyakimya ambako alikuta tayari kuna gari nje inamsubiri huku mama yake akitolewa mlango wa kawaida kisha kukutana nje na haraka gari hiyo ikaondoka kwa kasi kutoka uwanja huo wa Kimataifa wa Julius Nyerere 3.


“Watu wengi walikuwa wanamsubiri pale wanapotokea abiria wakiwemo waandishi lakini KI akatolewa mlango wa watu maarufu akiwa na hao watu wawili na mama yake akatokea mlango wa kawaida kisha kukutana pale nje akikuta tayari KI alikuwa ndani ya hiyo gari, hapo ndipo walipofanikiwa kutukimbia,“ alisema afisa huyo.


Jana asubuhi saa tano mshambuliaji huyo alikutana na uongozi wa juu wa Yanga akiwemo Rais wa klabu hiyo, injinia Hersi Said kisha baadaye kuanza taratibu za utambulisho.


Hersi ndio kigogo aliyemsainisha KI akiwa nchini Ivory Coast kama ambavyo Mwanaspoti lilivyokuwa linakuletea mfululizo wa habari za usajili huo kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Rasmi sasa KI anakuwa staa wa tano raia wa kigeni kusajiliwa na Yanga kuelekea msimu ujao akitanguliwa na mshambuliaji Mzambia Lazarous Kambole, kiungo mshambuliaji Bernard Morrison raia wa Ghana, kiungo mkabaji Mrundi Gael Bigirimana na beki Mkongomani, Joyce Lomalisa.

Post a Comment

0 Comments