Ticker

6/recent/ticker-posts

Gael Bigirimana Mashabiki Yanga Mtafurahi

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KIUNGO mpya wa Yanga, Gael Bigirimana amesema katika mahojiano maalumu kilichomleta Jangwani, huku akisema kwa kushirikiana na wenzake, makombe hayatakauka kwa namna watakavyoipigania timu na kuwapa furaha mashabiki wao.


Kiungo huyo wa zamani wa Newcastle United ya England, alisema amekuja Yanga kufanya kazi ikiwa ni mipango yake ya muda mrefu kurudi kucheza Afrika na aliondoka akiwa ni mdogo.

“Nimekuja Yanga kutokana na historia na ukubwa wa timu hii, nimekuwa nikiisikia kwani ni klabu kubwa Afrika na wachezaji wengi wa Afrika hususani ukanda wetu wanatamani kucheza hapa,” alisema Bigirimana na kuongeza;

“Mimi sio mchezaji wa kwanza kucheza Ulaya na kurudi Afrika na sitakuwa wa mwisho. Binafsi huko nimecheza kwa uwezo wangu na kila mtu ameona sasa ni zamu ya kucheza ndani ya bara langu kwani ni miaka mingi nimekuwa Ulaya,” alieleza Bigirimana.

Nyota huyo anayemudu kucheza maeneo yote ya kiungo hususani kiungo wa chini na kati alisema ujio wake ndani ya Yanga umelenga kutwaa makombe mbalimbali ambayo timu hiyo itashiriki na kuwapa furaha mashabiki wake.

“Kikubwa ni kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunashinda makombe tutakayoshiriki, pili kuifanya Yanga iwe timu inayoheshimika zaidi Afrika. Wachezaji waliopo ni bora na mimi ni bora hivyo tukiungana kwa pamoja naamini tutatengeneza timu tishio,” alisema Gael aliyewahi kuichezea timu ya taifa ya England U-20 kabla ya kuamua kuichezea Burundi.

Rais mpya wa Yanga, Hersi Said wakati wa utambulisho wa Bigirimana alieleza ni malengo yao kuweka heshima kwenye soka la Afrika ndio maana wanasajili wachezaji bora na wenye historia kubwa.

“Huyu tumetoa England, sio mchezaji wa kawaida na tunafanya hivi ili kuijenga Yanga ya kuheshimika na itakayobeba makombe makubwa ndani na nje ya nchi,” alisema Hersi.

Bigirimana amesaini Yanga kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Glentoran FC ya Ligi Kuu Ireland na kabla ya hapo alizichezea Solihull Moors ya England, Hibernian FC, Motherwell FC na Rangers za Scotland, na Conventry, Newcastle za England.

Post a Comment

0 Comments