Ticker

6/recent/ticker-posts

Erik ten Hag Aendelea Kumshawishi Cristiano Ronaldo Kubaki Manchester United

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


KOCHA wa Manchester United  Erik ten Hag anaendelea kumshawishi nyota Cristiano Ronaldo asiondoke, ingawa Mreno huyo mwenye umri wa miaka 37 amesisitiza kwamba angependa aruhusiwe aondoke kabla ya msimu mpya kuanza.

Nyota huyo hakuweza kujiunga na wenzake mazoezini nchini Thailand na Australia kwa madai ya sababu za kifamilia.

Hakuwepo kikosini tangu msimu umalizike, lakini amerejea kwa mazungumzo hayo ya dharura, baada ya Ten Hag kudai kwamba anamhitaji kwenye mipango yake ya msimu ujao.

Ronaldo alirejea United msimu uliopita, baada ya kuchezea Real Madrid na Juventus misimu ya hapo awali.

Ten Hag alisema amezungumza na Ronaldo kabla ya ziara ya Thailand na Australia, akieleza: “Yalikuwa mazungumzo ya kufana. Tuliyozungumza ni siri yangu na yeye. Ninachoweza kusema hapa ni kwamba tulikuwa na mazungumzo ya kufana pamoja.”

Kukosekana kwa Ronaldo ziarani Thailand na Australia kulizua uvumi kuhusu hali yake ya baadaye, siku chache tu baada ya kukosa kuingia mazoezini Carrington, huku kukiwa na madai kwamba alikuwa akifanya mazoezi na kikosi cha timu ya taifa.

Ronaldo ambaye amebakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake alikuwa mfungaji wa mabao mengi wa United kwa msimu uliopita na kushika nafasi ya tatu kwa wafungaji bora kwenye Ligi kuu, ingawa uchezaji wa kikosi hicho kwa Ujumla haukuridhisha mashabiki.

United walimaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza (EPL), hivyo kukosa nafasi ya kufuzu kwenye michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya, na sasa itabidi acheze michuano ya Europa League iwapo atakubali kuendelea kuwepo Old Trafford.

Nyota huyo ambaye ni mshindi mara tano wa Ballon d’Or anaonelea kuna klabu nyingi zenye uwezo wa kumnunua ili acheze katika mechi za Klabu Bingwa msimu ujao, badala ya Europa League ambayo ni ya hadhi ya chini.

Chelsea ambayo ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikitaka kumnasa ilikata tamaa mapema mwezi huu, na sasa huenda akaamua kujiunga na Bayern Munich au Atletico Madrid, ingawa United imesisitiza kwamba haendi popote kwa sasa.

United itakutana na Atletico Madrid nchini Norway Jumamosi, kabla ya kucheza mechi ya mwisho ya kupimana nguvu dhidi ya Rayo Vallecano Old Trafford Jumapili.

Mechi yao ya kwanza kwenye msimu mpya wa ligi kuu itakuwa dhidi ya Brighton mnamo Agosti 7.

Post a Comment

0 Comments