Ticker

6/recent/ticker-posts

NAMNA LIVERPOOL WANAMVYOMKUMBUKA MANE

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

 

STORI ya kusisimua mchana wa Agosti 14, 2016, ugenini Emirates dhidi ya Arsenal, Liverpool tunaongoza 3-1 mbele ya wenyeji.

Philippe Coutinho akiwa amefunga mabao mawili, Adam Lallana moja. Ndani ya uwanja jezi namba 19 ya Liverpool imevaliwa na mchezaji mpya kikosini, Sadio Mane.

Mechi ya kwanza ya msimu, mechi ya kwanza kwa Sadio ndani ya jezi yetu akitokea kwa wasamaria wa Southampton.

Dakika ya 59, Jurgen Klopp anamuita Sadio, anamwambia: “Sadio hii ni mechi yako ya kwanza, funga bao uje nikubebe kwenye mgongo wangu.”

Fikiria kocha anamwambia mchezaji wake funga bao kisha ambebe.

Tuchepuke kidogo: Stori ya makocha wa Liverpool kuwabeba wachezaji wao siyo ngeni. Tuliona Bill Shankly kwenye utawala wake Liverpool akimbeba Emyl Hughes na akina Roy Clemence.

Tukaona nyakati za Bob Paisley akimbeba Alan Hansen, Kenny Dalglish na hata Ian Rush.

Lakini Bill na Bob wote waliwabeba wachezaji wao wakiwa wamepata majeraha.

Kutokea hapo, wamepita makocha wengi hawakuwabeba wachezaji. Siyo Roy Evans, Gerrard Houllier wala Rafael Benitez.

Turudi njia kuu; Stori ya kusisimua pale Emirates mchana ule wa Agosti 14, ni Klopp kutaka kumbeba Sadio Mane endapo atafunga bao.

Upendo wa namna gani huu kuwahi kuuona katika karne ya 21? Alex Ferguson aliwahi kumbeba nani pale Old Trafford katika utawala wake?

Jose Mourinho je? Siyo Pep Guardiola wala Carlo Ancelloti aliyewahi kufanya hivyo.

Tusogee hapa, Dakika ya 63, Sadio Mane anafunga bao zuri la jitihada binafsi na moja kwa moja anakimbia hadi alipo Klopp ambaye anageuza mgongo wake ambebe.

Hii haikuwa bahati mbaya, haya ni mapenzi binafsi ya Kocha kwa mchezaji wake.

Mchezaji ambaye msimu mmoja nyuma anaifunga Liverpool bao mbili akiwa na jezi ya Southampton na baada ya filimbi ya mwisho kulia Klopp anampatia kumbato lenye kuashiria kumuhitaji.

Tokea Klopp ambebe Sadio pale Emirates hajafanya hivyo kwa mchezaji mwingine yeyote.

Leo Sadio ametuaga mashabiki wa Liverpool, mashabiki alioishi nasi kwa misimu sita yenye machozi na uchungu, furaha na vicheko.

Misimu sita yenye mafanikio kwake binafsi na kwa Klabu, ni wakati mgumu mchezaji aina ya Sadio kuondoka, mchezaji tuliyempenda na kumtungia nyimbo nyingi za kusifu kipaji chake.

Rekodi zake ni kubwa, mabao yake ni mengi, sitosahau bao lake alilomfunga Manuel Neuer pale Allianz Arena mwaka 2019.

Mtoto kutoka Bambali ambaye jina lake lipo katika majina yale tuliyoyafukia pale Axa Training Center Kirby na yatafukuliwa 2070.

Majina ya wachezaji waliorudisha furaha ya Liverpool baada ya miaka 70. Jina la Sadio ni mojawapo na kwetu ameondoka akiwa Legend.

Mwandishi wa makala haya ni Beki Mchawi, Marco Mzumbe ndani ya Gazeti la Spoti Xtra.

You’ll Never Walk Alone Sadio Mane.

Post a Comment

0 Comments